KWA NINI TYSON FURY ALIVAA BENDERA YA NIGERIA MDOMONI?
Bondia Muingereza Tyson Fury alivaa ‘Mouth Shield’ yenye rangi za bendera ya Nigeria katika pambano lake aliloshinda dhidi ya Deontay Wilder Februari 23 Las Vegas.
Hii imepelekea baadhi ya watu kutafsiri kuwa Fury alikuwa anapeleka ujumbe wa kutaka pambano dhidi ya Anthony Joshua ambaye ana asili ya Nigeria.
Joshua katika bega lake la kulia amechora tattoo ya ramani ya nchi ya Nigeria na hivi karibuni alienda kusajili kitambulisho cha Taifa mjini Abuja.
Baada ya ushindi huo wa Fury, watu wengi wanataka kuona mechi ya muunganiko wa mikanda dhidi ya Anthony Joshua — Promota maarufu Eddie Hearn kutumia mtandao wake wa kijamii wa Instagram, aliandika kuwa sasa ni muda Fury kupigana na AJ, na hakuna haja ya Fury na Wilder kupigana kwa mara ya tatu
Hata hivyo Wilder ameanza kutibua mpango huo baada ya kusema kuwa anataka marudiano tena na Fury.
Wilder ambaye alipoteza pambano kwa mara ya kwanza katika mchezo huo wa ngumi, alijitetea kwa kusema kuwa nguo alizovaa kuingia nazo ulingoni zikiwa na uzito wa kilo 18—zilipelekea kupoteza pambano hilo.