TYSON FURY AMPIGA WILDER KWA TKO
Bondia wa Uingereza Tyson Fury ameshinda pambano lake la marudiano dhidi ya Deontay Wilder kwa TKO raundi ya 7 na kutangazwa kuwa bingwa mpya wa WBC wa uzito wa juu.
Pambano hili likipigwa MGM Grand, Las Vegas Marekani, lilikuwa pambano lililosubiriwa kwa hamu, Tyson Fury akisaka ushindi kwa nguvu baada ya kuona alinyimwa ushindi kwenye pambano la kwanza walilokutana mwaka 2018.
Fury alionekana kumshambulia Wilder kwa kasi toka raundi ya kwanza, na raundi ya tatu ndiyo ilibadilisha kila kitu baada ya kumpiga Wilder ngumi ya sikio na kumuangusha chini.
Huo ndio ulikuwa mwanzo wa kumaliza kebehi zote za Bronze Bomber.
Wilder,34,hakuweza kurejea tena mchezoni, raundi ya tano alijikuta tena chini na Fury kuanza kulamba utamu wa ushindi.
Raundi mbili baadae pambano halikuweza kuendelea, baada ya ngumi mfululizo alizorusha Fury kwa Wilder aliyekuwa kwenye kona, timu ya Wilder ikaamua kurusha taulo ulingoni na mwamuzi kumaliza pambano na ushindi kwenda kwa Fury.
Tyson Fury,31,ameandika historia ya kuwa bondia wa kwanza kushinda dhidi ya Deontay Wilder ambaye kabla ya pambano la leo alikuwa amepigana mapambano 43, akishinda 42 (41 kwa KO) na sare moja ambayo ilikuwa dhidi ya Tyson Fury mwaka 2018.
Tyson Fury amebaki na rekodi yake ya kutopoteza pambano mpaka sasa, akicheza mapambano 31, akishinda 30 (21 kwa KO) na sare moja.