EPL IMEENDELEA: BAADA YA KICHAPO UNAI EMERY AOMBA MUDA ZAIDI KUKUZA WATOTO
Ligi kuu ya England EPL imeendelea Novemba 9, zikichezwa jumla ya mechi 6
Mechi ya kwanza ilikuwa ni Chelsea dhidi ya Crystal Palace, Frank Lampard akiendelea pata matokeo mazuri kwa kikosi chake kuibuka na ushindi wa goli 2 – 0 zilizofungwa na Tammy Abraham 52′ na Pulisic 79′.

Katika uwanja wa King Power stadium, Leicester City wamefanikiwa ibuka na ushindi wa goli 2 – 0 dhidi ya Arsenal. Kocha wa Arsenal Unai Emery akihojiwa baada ya mechi alisema “Nia sasa ni kushinda mechi inayofuata dhidi ya Southampton na kuendelea hivo katika mechi 38.

Tunahitaji muda na kuwa wavumilivu. Tumebadilisha wachezaji wengi na wengi ni wadogo. Tumekuwa na mambo mengi ambayo hayajatusaidia kupata matokeo mazuri. Ila kwa kuwa wavumilivu na wenye stamina tutafanya vizuri.”
Matokeo haya yameendelea chochea vuguvugu la kufukuzwa kwa kocha huyu toka kwa mashabiki akiwa hajapata ushindi katika mechi ya nne.

Mechi nyingine ilikuwa ni kati ya Tottenham dhidi ya Sheffield United, mechi iliyoisha kwa sare ya goli 1 – 1. Mechi hii ilihusisha maamuzi ya VAR baada ya kukataliwa kwa goli la kusawazisha la Sheffield kwa madai ya mchezaji kuwa ameotea.

Mechi nyingine ilikuwa ni kati ya Burnley dhidi ya West Ham, Burnley akiibuka na ushindi wa goli 3 – 0. Newcastle wakiibuka na ushindi wa goli 2 – 1 dhidi ya Bournemouth na Everton wakiondoka na ushindi wa 2 – 1 ugenini dhidi ya Southampton.
Mechi nyingine zitaendelea kesho zikiwa ni kati ya Manchester United dhidi ya Brighton, Wolves dhidi ya Aston Villa na ile ya vita ya Ubingwa Liverpool dhidi ya Man City katika dimba la Anfield.