CLUB BRUGE YAMPIGA ADHABU MBAYE DIAGNE KWA KUKOSA PENATI DHIDI YA PSG
Msenegali Mbaye Diagne amepigwa faini na kuondoshwa katika kikosi cha Club Bruge ya Ubelgiji kwa kosa la kukosa penati katika mechi ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya PSG katika mechi iliyoisha kwa kupoteza 1 – 0 Jumatano iliyopita nchini Ufaransa
Akitokea benchi Diagne alifanyiwa madhambi yaliyosababisha penati na akachukua maamuzi ya kuipiga yeye mwenyewe, penati ambayo iliokolewa kirahisi na kipa Keylor Navas.

Kocha wa Club Bruge akiongea na wanahabari jana Ijumaa alisema “Hatotokea katika kikosi changu katika mchezo wa ligi dhidi ya Antwerp siku ya Jumapili, na nitaamua juu ya yeye kurejea kikosini wiki ama miezi ijayo. Na zaidi kutakuwa na adhabu kali ya kifedha.”
Kocha huyu aliweka wazi kuwa jukumu la kupiga penati katika timu yake ni la mchezaji Hanas Vanaken na sio Mbaye Diagne.

Club Bruge ambao wanaongoza ligi ya Ubelgiji, wanashika nafasi ya tatu katika kundi A la Klabu Bingwa wakiwa na pointi 2, PSG wakiwa na pointi 12 na Real Madrid Pointi 7. Mbaye Diagne hadi sasa amecheza mechi 13 za ligi msimu huu akifunga magoli manne.