ZAHERA ATIMULIWA YANGA
Mwenyekiti wa Yanga Mshindo Msolla leo ametangaza kuwafuta kazi kocha mkuu wa timu hiyo Mwinyi Zahera pamoja na benchi lake la ufundi .
Kocha wa zamani wa timu hiyo Boniface Mkwasa ndio ametangazwa kukaimu nafasi ya Zahera.
Zahera ambaye ana uraia wa DR Congo na Ufaransa, alijiunga na klabu ya Yanga katika msimu wa 2017/18, anaondoka Yanga ikiwa hazijapita saa 48 tangu timu hiyo itolewe na Pyramids FC katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Yanga imerejea nchini Tanzania jana mchana ikitokea nchini Misri, ambapo juzi Jumapili ilipoteza mechi dhidi ya Pyramids kwa goli 3-0 na kutolewa katika raundi hiyo ya mtoano kwa jumla ya goli 5-1, hii ni baada ya mechi ya nyumbani waliyocheza jijini Mwanza, kuisha kwa kufungwa goli 2-1.
Zahera anaondoka Yanga akiicha katika nafasi ya 18 katika VPL msimu huu, ambapo wamecheza mechi 4, wakishinda mbili, sare moja na kupoteza, wakiwa na jumla ya pointi 7.