AUBAMEYANG ARUDISHA MAJIBU KWA CEO WA DORTMUND
Mshambuliaji wa klabu ya Arsenal Pierre Emerick Aubameyang ameshindwa kumlazia damu Afisa mtendaji mkuu wa klabu yake ya zamani Borussia Dortmund Hans-Joachim Watzke, aliyedai kuwa mchezaji huyo aliondoka klabuni hapo kwa ajili ya kwenda kufuata pesa Arsenal.
Watzke akizungumza na gazeti la Ujerumani, Suddeutsche Zeitung mapema wiki hii alisema :” Wengine huenda katika klabu kwa ajili ya hizi pesa, ambapo hawachezi Klabu Bingwa kwa miaka.
Aubameyang, ambaye anacheza vizuri Arsenal, atakuwa anafurahia anapoangalia akaunti yake ya benki, lakini katika siku za Jumatano atakuwa mwenye huzuni pale anapotakiwa kuangalia Klabu Bingwa kwenye Televisheni.”
Baada ya kusikia hayo, Aubameyang jana ameamua kumjibu Watzke akimuita ni kikaragosi.
Kupitia ukurasa wake wa Twitter Aubameyang aliandika : “ Ni kheri kwako sijawahi kuongea ni kwa nini hasa niliondoka Dortmund Mr Watzke, wewe ni kikaragosi.
Ninakumbuka kipindi kile ulisema hatutomuuza Ousmane (Dembele), kisha ulipoona zaidi ya Milioni 100 ulikuwa wa kwanza kuchukua zile pesa. Usiongee kuhusu pesa tafadhali !!!!! Niache peke yangu tafadhali.”
Dortmund ilimuuza Dembele kwenda Barcelona mwaka 2017 kwa ada inayoongezeka mpaka Pauni 135, licha ya awali Watzke kuahidi winga huyo hatauzwa.
Aubameyang,alijiunga na Arsenal Januari 2018 kwa ada ya Pauni milioni 56 akitokea Dortmund alipocheza tangu mwaka 2013.