FIFA YATAKA CARDIFF KULIPA PESA ZA USAJILI WA SALA
Shirikisho la soka Duniani FIFA limeagiza klabu ya Cardiff iwalipe Euro milioni 6 (Pauni mil 5.3) klabu ya Nantes juu ya usajili wa mshambuliaji Emiliano Sala.
Mchezaji huyo,28,alifariki kwa ajali ya ndege Januari 21 akiwa safarini kutoka Ufaransa kwenda Uingereza tayari kuanza kazi katika klabu ya Cardiff.
FIFA imewataka Cardiff kutoa malipo hayo, ambayo ni malipo ya awali kama klabu hizo zilivyokubaliana katika usajili wa Muargentina huyo.
Nantes walimuuza Sala kwa ada ya Pauni milioni 15 kwenda Cardiff, na timu hizo zilikubaliana malipo yafanyike katika awamu tatu.
Cardiff walisema kuwa Sala hakuwa mchezaji wao rasmi na hivyo hawataweza kulipa hela yoyote ya usajili wa mchezaji huyo.
Klabu hiyo ilidai kuwa mkataba wao na Sala haukuwa bado na makubaliano ya kisheria na hivyo kukataliwa na ligi kuu nchini England kwa kuvunja kanuni za usajili.
Timu zote Cardiff na Nantes wamepewa chaguzi za kukata rufaa juu ya maamuzi hayo katika mahakama ya michezo ya kimataifa (CAS)
Bado haijawekwa wazi na FIFA kama Cardiff watatakiwa kulipa malipo mengine mawili ya usajili huo kama ilivyokuwa imepangwa hapo mwanzo.