RAIS WA FUFA KWENYE KASHFA NZITO YA KUUZA TIKETI ZA KOMBE LA DUNIA 2014
Rais wa shirikisho la soka nchini Uganda (FUFA) Moses Magogo ameingia katika kashfa nzito ya uuzaji wa tiketi za Kombe la Dunia 2014 kinyume na taratibu walizoelekeza FIFA.
Magogo akiwa katika mkutano mkuu wa FUFA ametangaza kujiweka pembeni kwa miezi miwili kupisha uchunguzi na nafasi yake itachukuliwa na makamu wa kwanza wa Rais wa FUFA Justus Mugisha.
Magogo ametangaza maamuzi hayo katika mkutano mkuu wa FUFA wa 95 uliyofanyika Adjuman,juzi Jumamosi Septemba 28.
Kesi ya uuzwaji wa tiketi ya Magogo ilipelekwa FIFA na mwandishi wa habari za michezo na Mbunge wa jimbo la Makindye Magharibi nchini Uganda ambaye pia ni waziri kivuli wa michezo Allan Ssewanyana kuwa hakufuata taratibu kugawa tiketi hizo.
Kesi hiyo ilipelekwa FIFA Mei 30 2017 katika kamati ya maadili ya FIFA ikimtuhumu Magogo kuuza tiketi 177 nje ya Uganda tofauti na ilivyoelekeza FIFA hiyo ni kwa mujibu wa Ssewanyana
Kawaida katika kila fainali ya Kombe la Dunia FIFA hutoa tiketi hizo kwa mashirikisho yote ya soka kwa idadi fulani iwauzie raia wake lakini inadaiwa magogo hakufanya hivyo.