MARIGA KAINGIA KWENYE SIASA RASMI TUMSUBIRI NOVEMBA 7 2019
Kiungo wa zamani wa klabu ya Inter Milan na Parma za Italia raia wa Kenya McDonald Mariga ameingia rasmi kwenye ulingo wa siasa baada ya kutangazwa kama mgombea wa jimbo la Kibra nchini Kenya.
Bodi ya taifa ya uchaguzi nchini Kenya (NEB) chini ya mwenyekiti wake Andrew Musangi baada ya kumuhoji na kujiridhishwa ametangazwa mgombea wa Ubunge wa Jimbo la Kibra kupitia chama cha Jubilee ambapo aliwashinda wagombea wengine 16 waliokuwa wanawania ridhaa ya kugombea jimbo hilo katika uchaguzi wa mdogo Novemba 7 2019.
Uchaguzi huo unafanyika baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo,Ken Okoth kufariki dunia kwa ugonjwa wa Kansa Julai,26,2019.
Mariga ambaye ameandika historia ya kuwa mchezaji wa kwanza wa Kenya kucheza Michuano ya Klabu Bingwa Ulaya na kuwa mchezaji pekee Afrika Mashariki aliyetwaa medali ya michuano hiyo, kama atafanikiwa kutwaa nafasi hiyo ataungana na Rais wa Liberia George Weah aliyewahi kuwa mchezaji wa AC Milan na baada ya kustaafu aliingia kwenye siasa na kugombea Ubunge na baadae Urais.