FORLAN AELEZA KIUNDANI KUHUSU UGOMVI WA FERGUSON NA BECKHAM 2003
Moja ya tukio maarufu katika soka mwaka 2003 lilikuwa ni ugomvi uliotokea kwenye vyumba vya kubadilishia vya Old Trafford.
Ugomvi huu ulikuwa ni kati ya kocha wa Man United wakati huo, Sir Alex Ferguson na mchezaji wake David Beckham ambao ulitokea baada ya Man United kupoteza mechi ya raundi ya 5 FA Cup kwa bao 2-0 dhidi ya Arsenal
Miezi michache baada ya ugomvi huo, Sir Alex alimuuza Beckham kwenda Real Madrid kwa ada ya Pauni milioni 25.

Diego Forlan ambaye alikuwa Man United katika kipindi hicho, katika mahojiano na gazeti la Daily Mirror hivi karibuni ameelezea kilichotokea katika ugomvi huo.
“Ilikuwa ni baada ya mechi dhidi ya Arsenal katika FA Cup na Ferguson hakuwa na furaha kwa sababu Robert Pires alipita upande wa kushoto, Gary Neville alikuwa mbali, na Beckham hakurudi kuja kuziba”
“Katika vyumba vya kubadilishia nguo, Ferguson na Beckham walianza kutukanana. Kila tusi lilikuwa kubwa zaidi ya lililopita na wanaume wote walitaka kuwa na neno la mwisho.
Baadae Ferguson akaondoka na kuonekana ule mjadala umekwisha, lakini mara Beckham akasema kitu kingine. Ferguson aligeuka na kuona kiatu chini na kukipiga kuelekea kwa Beckham.Kichuma kikubwa kikampiga (Beckham) kwenye nyusi.
“Wote tukaona damu. Baada ya muda mchache wakaanza kutaka kupigana. Hapo ndipo Roy Keane na Van Nistelrooy wakaingia na kuwatenganisha.”