Mwanamitindo amponza nyota wa Misri
Uongozi wa timu ya taifa ya Misri mapema jana kabla ya mchezo na DR Congo walifikia maamuzi ya kumuondoa kikosini nyota wao Amr Warda.
.
Warda anayekipiga PAOK ya Ugiriki anaondolewa katika kikosi cha AFCON cha Misri baada ya kucheza mchezo mmoja, hiyo ni baada ya mwanamitindo mwenye asili ya Misri na Uingereza Merhan Keller kuonesha hadharani meseji zisizofaa na za shari za kimapenzi alizokuwa anatumiwa na winga huyo kupitia Instagram na WhatsApp.
Baada ya mwanamitindo huyo kutoa meseji hizo,wanawake wengine nao waliibuka na kuonesha meseji kama hizo walizotumiwa na mchezaji huyo, huku wengine wakionesha picha na video za utupu alizokuwa anatuma ili kuwashawishi kimapenzi.
Meseji zilionesha jinsi ambavyo Warda alikuwa anakuwa mbogo pale anapokataliwa, alikuwa akiwatumia meseji za vitisho ili akubaliwe.
Hii si mara ya kwanza Warda kukutana na shutuma kama hizo, mwaka 2017 klabu ya Ureno Feirense ilikatiza mkataba wa mkopo na mchezaji huyo ikiwa haijaisha wiki moja tangu ajiunge na nayo, iliripotiwa kuwa mkataba huo ulisitishwa baada ya Warda kudaiwa kuwanyanyasa kijinsia wake wawili wa wachezaji wenzake katika timu hiyo.
Baada ya kutolewa kwenye kikosi,Misri ambayo tayari imefuzu hatua ya mtoano sasa imebaki na wachezaji 22.