Mchezaji wa Czech afariki kwa ajali ya gari
Mchezaji wa kimataifa wa Jamhuri ya Czech Josef Sural amefariki dunia baada ya gari dogo alilokuwa amepanda na wachezaji wenzake wa Aytemiz Alanyaspor kupata ajali wakiwa wanarejea nyumbani kutoka kucheza mechi ugenini huko nchini Uturuki.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa klabu,dereva wa gari hiyo alisinzia wakati anaendesha na hivyo kupelekea ajali iliyosababisha kifo cha Sural,28,ambaye alifariki Hospitali ambapo wachezaji wenzake sita nao walifikishwa baada ya kujeruhiwa.
Mwenyekiti wa klabu Hasan Cavusoglu alisema dereva alisinzia akiwa anaendesha, na dereva msaidizi wakati huo alikuwa amelala.
Gari hilo lilibeba wachezaji saba wa Alanyaspor ya huko Turkey akiwamo mchezaji wa zamani wa England Steven Caulker na mchezaji wa zamani wa Newcastle Pappis Demba Cisse wakitokea kucheza mechi ya ugenini dhidi ya Kayserispor iliyoisha kwa sare ya 1-1.