Nyota wa Burundi afia uwanjani Swaziland
Ulimwengu wa soka umezipokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha nyota wa zamani wa timu ya Bidvest ya nchini Afrika Kusini na timu ya taifa ya Burundi Papy Faty aliyefariki dakika ya 15 ya mchezo akiitumikia timu yake ya Malanta Chiefs ya Swaziland dhidi ya Green Mamba jana April 25.
.
Papy Faty ambaye ana umri wa miaka 28 amefariki mwanzoni mwa mchezo baada ya kuanguka katika uwanja wa Killarney na kukimbizwa hospitali na baadae taarifa kuthibitika kuwa Papy Faty amepoteza maisha.
.
Hii sio mara yake ya kwanza kuanguka uwanjani iliwahi kumtokea mara mbili akiwa na Bidvest mazoezini na kwenye mechi.
.
Baada ya Papy Faty kufanyiwa uchunguzi aligundulika ana tatizo la moyo na mwaka 2016 kushauria astaafu kucheza mchezo wa mpira wa miguu ili kulinda maisha yake, alistaafu na baadae kuamua kurudi tena uwanjani na kufuta uamuzi wake wa kustaafu mchezo huo.
.
Papy Faty anakuwa mchezaji wa nne wa kiafrika kuanguka na kufia uwanjani , baada ya Dominic James wa St George ya nchini Ethiopia 2016, Cheick Tiote akiwa mazoezini na timu yake ya Beijing Enterprises 2017 na Marc Vivien Foe 2003 akiwa na timu yake ya Cameroon katika mchezo wa mabara dhidi ya Colombia huku Fabrice Muamba wa Bolton akitangaza kustaafu soka mapema akiwa na umri wa miaka 24 baada ya kubainika kuwa na tatizo hilo 2012.