Ronaldo hatihati kuwakosa Ajax Klabu Bingwa
Shirikisho la soka Barani Ulaya UEFA limemshitaki nyota wa Juventus Cristiano Ronaldo kufuatia ushangiliaji wake baada ya ushindi wa 3-0 dhidi ya Atletico Madrid wiki iliyopita,ambapo alionekana akishangalia kwa kumuigiza kocha wa Atletico Madrid Diego Simeone katika mchezo wa kwanza walipokutana katika raundi hiyo ya 16 bora Klabu Bingwa Ulaya.
Sasa shirikisho hilo linaendelea kufanya uchunguzi na wametoa taarifa kuwa, watashughulikia kesi hiyo katika kikao chao kijacho Machi 21,2019.
Bado haijafahamika kuwa mchezaji huyo kama atafungiwa mchezo au atapewa adhabu gani, Simeone baada ya kufanya hivyo hakufungiwa mechi ila alipigwa faini.
.
“Ninafikiri kila mmoja anashangilia kwa njia yake uwanjani na jukwaani. Sikuona cha ajabu, ni ushangiliaji tu. Hakutakuwa na kifungo” amesema kocha wa Juventus Massimiliano Allegri baada ya UEFA kutoa taarifa hiyo.
Juventus katika hatua ya robo fainali kwenye michuano ya klabu bingwa Ulaya wanataraji kukutana na Ajax, mechi ya kwanza itachezwa Uholanzi April 10.