Gigi Buffon alimkatalia Ferguson kuja Man United mara 3
Mlinda mlango wa klabu ya Paris Saint Germain ya nchini Ufaransa Gianluigi Buffon ameeleza ukweli kuwa hakuwa na dhamira au nia ya kucheza Ligi Kuu ya nchini England kwani amewahi kupata ofa mara kadhaa kutoka katika vilabu viwili vya Ligi hiyo lakini alikataa.
Buffon mwenye umri wa miaka 41 kwa sasa , ameichezea Juventus ya nchini kwa Italia kwa miaka takribani 17 toka alipojiunga 2001 akitokea Parma, ila kwa sasa amesaini mkataba wa mwaka mmoja kuichezea Paris Saint German ambayo ndio timu yake ya kwanza kucheza katika maisha yake ya soka iliyopo nje ya Italia.

Mlinda mlango huyo ameeleza kuwa kocha wa zamani wa Manchester United Sir Alex Ferguson alishawatuma maskauti mara tatu wamuangalie wamsajili akiwa Parma lakini alikataa , na Manchester City pia wakati wanaunda kikosi chao upya walimtaka na akawakatalia.
“Nilipokuwa mvulana mdogo ninaichezea Parma, Ferguson (Sir Alex) alinitaka kunisajili katika kipindi cha miaka miwili au mitatu tofauti na siku zote alikuwa akiwatuma maskauti waje kuniangalia lakini kwa wakati ule Parma ndio ilikuwa dunia yangu na sikuwa najisikia kama kuondoka” alisema Buffon akihojiwa na BT Sport
“Baadae nikapata ofa kubwa kutoka Manchester City wakati walipokuwa wanaanza kujenga timu yao na kufanya moja kati timu bora Ulaya, walinitaka niwe mchezaji wa kwanza kusaini kwao lakini niliamua kubakia Juventus” alisema Buffon katika mahojiano yake na BT Sport
Tukukumbushe tu Buffon aliyecheza mchezo wake wa kwanza wa timu ya wakubwa ya Parma Novemba 19 1995 dhidi ya AC Milan, ameichezea timu yake ya taifa ya Italia jumla ya michezo 176 na kutwaa Kombe la Dunia 2006, ngazi ya klabu Buffon amecheza michezo 405 bila kuruhusu nyavu zake kuguswa kati ya michezo 895 ya michezo .