Aussems azitaka pointi 3 kwa Lipuli
Klabu ya Wekundu wa Msimbazi Simba leo watakuwa mjini Iringa kuendeleza mbio zao za kutetea taji lao la Ligi Kuu dhidi ya Lipuli FC, mchezo ambao utachezwa katika uwanja wa Samora mkoani hapo, Simba wanatazamiwa kupata matokeo katika mchezo huo licha ya mchezo huo kutarajiwa kuwa na ushindani.
Meneja wa timu hiyo alithibitisha kuwa kikosi chao kipo kamili na wanamkosa mchezaji mmoja pekee Shomari Kapombe ambaye bado anaendelea kuuguza jeraha lake, kikosi cha Simba kimefanya mazoezi yake ya mwisho kabla ya kukipiga na Lipuli FC na kocha wao Patrick Aussems aliongea na Azam TV kueleka mchezo huo.
“Kundi lote tumekuta uwanja ni mzuri kwa hiyo tutakuwa na uwezo wa kucheza tunajua utakuwa ni mchezo mgumu kwa sababu timu hii imepata sare miezi michache iliyopita na mwaka jana Simba haikupata ushindi dhidi ya Lipuli, kwa hiyo ni wapinzani wagumu kwetu lakini tulikuwa na kiwango kizuri wiki iliyopita kwa hiyo tunahitaji kushinda na tuko tayari” alisema Patrick Aussems alipoongea na Azam TV kutokea Iringa
Simba sasa wapo nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania bara msimu wa 2018/2019 wakiwa na jumla ya alama 45 walizovuna katika michezo 18 ambapo pia bado wana viporo michezo saba kabla ya kukipiga na Lipuli FC ukilinganisha na wapinzani wao Yanga wanaoongoza Ligi kwa kuwa na alama 61 wamecheza michezo 25 sawa na Azam FC waliopo nafasi ya pili wakiwa na alama 50.