Wenger alimtabiria Mbappe
Kocha wa zamani wa klabu ya Arsenal ambaye aliondoka katika timu hiyo baada ya kudumu nayo kwa miaka 22, Arsene Wenger amenukuliwa na mtandao wa ESPN UK akisifia uwezo wa mchezaji wa kimataifa wa Ufaransa anayekipiga katika klabu ya Paris Saint Germain Klylian Mbappe.
Wenger amekiri kuwa alitambua kipaji cha Kylian Mbappe mapema kabisa kwa mara ya kwanza tu alivyomuona akicheza na kusema kuwa kwa sasa na sisi Ufaransa tumepata Pele wetu, yaani ni kama alitoa kauli ya kumtabiria makubwa kinda huyo kiasi cha kumlinganisha na mkongwe nwa Brazil Pele ambaye alikuwa na uwezo mkubwa na mahiri sana enzi zake.
“Kwa mara ya kwanza Napata nafasi ya kumuona Kylian Mbappe akicheza soka, nilisema ndio sasa Ufaransa tumempata Pele wetu” alisema Arsene Wenger alipozungumzia uwezo na umahiri wa Kylian Mbappe akiwa uwanjani.
Kocha Arsene Wenger ambaye amekiri kuwa hana uhakika kama atarudi katika kazi ya ukocha kama kawaida, alidumu na Arsenal kwa miaka 22 toka alipojiunga nayo 1996 akitokea Nagoya Grampus Eight na 2018 alimwaga manyanga kwa kujiuzulu kwa mwenendo mbovu wa timu yake ila ameweka rekodi mwaka 2004 ya kuwa kocha pekee aliyewahi kutwaa taji la Ligi Kuu England pasipokupoteza mchezo hata mmoja.