Haji Mnoga aikataa Tanzania
Waswahili wanasema nyota njema huonekana asubuhi lakini hii inaweza ikawa dalili njema kwa Haji Mnoga ambaye ni Muingereza mwenye asili ya Tanzania visiwani Zanzibar lakini amepata nafasi ya kuichezea timu ya taifa ya England, hii ni furaha kwake kutokana na kupata nafasi hiyo lakini ni pigo kwa Tanzania.
Haji Mnoga ambaye ni beki, anaichezea klabu ya Portsmouth ya nchini England amepata nafasi ya kuichezea timu ya taifa ya England ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 siku ya Februari 10 kama mchezaji wa England, hivyo aliamua kuutumia ukurasa wake wa instagram kueleza furaha yake ya kuichezea England.
“10/02/2019 ilikuwa mara yangu ya kwanza kuichezea England kitu ambacho najivunia mimi na familia yangu, kuwa na timu ya England kwa wiki nzima ni kitu cha kuvutia na kupata uzoefu mpya ni heshimu kubwa kwangu kuvaa jezi na England na kuitumikia ninaimani mengi yanakuja mbeleni” aliandika Haji Mnoga
Kimsingi Haji Mnoga ambaye alizaliwa mwaka 2002 Portsmouth Uingereza baba yake akiwa na asili ya Tanzania (Zanzibar) na mama yake akiwa muingereza kwa sasa ni muingereza kutokana na kuzaliwa huko ana haki ya kuichezea timu ya taifa ya nchi hiyo, hata hivyo hiyo inaonesha kama kuwasikitisha baadhi ya watanzania lakini anayo nafasi ya kuja kuchezea timu ya taifa ya Tanzania siku moja kama ataamua kubadili mawazo njiani, kutokana na sheria za FIFA kwa mchezaji mwenye asili ya mataifa mawili ana uwezo kucheza U-17, U-20, U-21 akiwa na taifa jingine lakini baadae katika timu ya wakubwa akabadili mawazo na kucheza taifa jingine ambalo ana uraia nalo.