Ndege aliyokuwa amepanda Emiliano Sala yapatikana
Baada ya nyota mbalimbali wa soka na watu mbalimbali kuchangia mchango wa kuendesha upya zoezi la kuwatafuta nyota wa Cardiff City Emiliano Sala na rubani wake Davis Ibbotson waliyokuwa wamepotea na ndege ndogo kwa zaidi ya wiki sasa wakitokea Nantes Ufaransa kurudi Cardiff Wales , jitihada zimezaa matunda za zoezi hilo la pili.
Awali Mamlaka za uokoaji baada ya kutafuta kwa zaidi ya saa 80 ndege hiyo iliyokuwa inahisiwa kuanguka katika fukwe za Guernsey, walikata tama na kutangaza kusitisha zoezi hilo ndipo watu mbalimbali walipoamua kuchanga na kulipia gharama za kuendelea kumtafuta Emiliano Sala na rubani wake ambapo ndege yao ndogo ilipotea kwenye rada toka Januari 21 2019, familia tayari zimepewa taarifa za kuonekana kwa ndege hiyo.
Usiku wa Jumapili ya Februari 3 baada ya zoezi hilo kufanyika ndege hiyo imefanikiwa kuonekana lakini Emiliano Sala na rubani wake wakiwa bado hawajapatikana, kwa hali ilivyo wanahisiwa kupoteza maisha, japokuwa zoezi la utafutaji bado linaendelea.
Sala alipata ajali hiyo akiwa njiani kurejea Cardiff aliyokuwa kajiunga nayo siku mbili nyuma akitokea Nantes ila siku hiyo alikuwa anatoka Nantes alipokuwa kaenda kuwaaga wachezaji wenzake baada ya kukamilisha uhamisho wa pauni milioni 15.