Hatimaye Solskjaer aonja ugumu wa EPL Man United
Mara nyingi wanaoitaja Ligi Kuu nchini England kuwa bora barani Ulaya zaidi ya Ligi nyingine ni kutokana na Ligi hiyo kuwa na ushindani mkubwa ukilinganisha na Ligi nyingine Ulaya, Uingereza pekee ndio Ligi ambayo huwezi kujua Bingwa nani hadi imalizike au kabla ya mechi tatu kabla ya Ligi kuisha wakati Ligi nyingine ni rahisi mwezi Desemba kufika ukaanza kujua kabisa flani atakuwa Bingwa.
Baada ya kuishi maisha ya raha na burudani kama kocha wa Manchester United Ole Gunnar Solskjaer, nusuru acheze kichapo akiwa nyumbani Old Trafford akicheza dhidi ya Burnley, waliyoonekana kuja kutaka kuvuruga rekodi ya Solskjaer aliyoweka ya kuiongoza Manchester United katika michezo nane ya kwanza pasipokupoteza mchezo hata mmoja wala kusuluhu,
Manchester United wamejikuta wakilazimishwa sare nyumbani na timu ya Burnley iliyopanda hadi nafasi ya 15 katika msimamo wa Ligi Kuu England baada ya Barnes dakika ya 51 na Chris Wood dakika ya 81 kufunga mabao ya uongozi kwa Burnley ila baada ya Manchester United kuongeza presha wakajikuta wakipata penati dakika ya 87 na Paul Pogba kufunga, ndipo dakika mbili za nyongeza Lindelof akainusuru Manchester United na aibu ya kufungwa nyumbani kwa kufunga bao la kusawazisha.
Solskjaer sasa atakuwa na wakati mgumu wa kuanza kuthibitisha ubora wake, kwani maneno ya mtandaoni yanadai kuwa wachezaji wa Manchester United walicheza kwa nguvu mno mechi 8 za mwanzo ili kuonesha kuwa Jose Mourinho ndio alikuwa tatizo kwani inaonekana walikuwa hawamuhitaji.
Kwa mara ya kwanza toka Manchester United iwe chini ya Ole Gunnar Solskjar ndio imepoteza alama , hivyo sare hiyo bado inawaweka katika wakati mgumu wa kumaliza TOP 4, Manchester United baada ya sare ya 2-2 katika msimamo wa Ligi Kuu ya nchini England wapo nafasi yao ile ile ya sita wakiwa na alama 45 tofauti ya alama 2 na Arsenal aliyopo nafasi ya tano.