FABREGAS ANAONDOKA UINGEREZA BAADA YA MECHI 501
Kiungo wa timu ya Chelsea Cesc Fabregas raia wa Hispania leo amebubujikwa na machozi mbele ya mashabiki wa Chelsea waliokuwa wamejitokeza katika uwanja wao wa Stamford Bridge kutazama mechi ya FA Cup ya Chelsea dhidi ya Nottingham Forest iliyomalizika kwa Chelsea kushinda mabao 2-0.
Cesc Fabregas mwenye umri wa miaka 31 hiyo ilikuwa ni mechi yake ya mwisho akiwa Stamford Bridge hivyo aliitumia kuwaaga mashabiki huku akitokwa machozi ila inaarifiwa kuwa nyota huyo yuko mbioni kwenda kuungana na nguli wa Arsenal Thierry Henry katika kikosi anachokinoa cha AS Monaco cha nchini Ufaransa.
Fabregas ambaye alikuwa nahodha wa Chelsea katika mchezo huo anaondoka Uingereza akiwa kacheza jumla ya michezo 501 akicheza katika soka la Uingereza akiwa na Arsenal na Chelsea kwa nyakati mbili tofauti, Fabregas alitoka uwanjani analia nafasi yake ikichukuliwa na Ng’olo Kante huku akiwaaga mashabiki.

Kiungo huyo mahiri anaondoka Chelsea baada ya kudumu nayo kwa miaka minne toka alipojiunga nayo mwaka 2014 akitokea FC Barcelona lakini ameichezea pia mechi 198 katika mashindano yote toka ajiunge nayo na kufunga mabao 22.
“Muda unakwenda najihisi kama ni wiki iliyopita ndio nimeanza kucheza soka la kulipwa lakini sasa ni zaidi ya miaka 15 nacheza soka la kulipwa, miaka inaenda haraka sana katika soka inatakiwa uwe stand by kila baada ya siku tatu, kwa ukosoaji wa kila mmoja, watu kusifia ubora wako na kupanda na kushuka kwa hapa na pale”alisema Cesc Fabregas