KOCHA WA SIMBA KAWATUPIA LAWAMA WACHEZAJI KUTOLEWA NA MASHUJAA FC
Kwa mara ya pili mfululizo Simba SC inakumbana na janga la kuondolewa katika michuano ya Kombe la Azam Sports Federation Cup hatua za mapemda dhidi ya timu ya daraja la chini, Simba SC siku ya Boxing Day ilicheza dhidi ya timu ya Mashujaa kutoka Kigoma na kupoteza.
Simba ambao wamefuzu hatua ya makundi kucheza michuano ya klabu Bingwa Africa licha ya kuitoa Nkana FC kishujaa katika michuano ya klabu Bingwa Afrika mzunguuko wa kwanza, wameshindwa kuitoa timu ya daraja la chini katika michuano ya Azam Sports Federation Cup, Simba imeondolewa katika michuano hiyo kwa mabao 3-2, bao la tatu la Mashujaa likifungwa dakika za lala salama.
Hata hivyi baadhi ya watu kufuatia kipigo hicho lawama zimemuangukia kocha wao Patrick Aussems kwa kusema kuwa angepanga kikosi cha kwanza lakini, wengine wanamlaumu mlinda mlango wao namba 2 Deogratus Munish Dida kwa kuruhusu kufungwa bao la tatu likidaiwa la kizembe, hata hivyo baada ya mchezo Kocha wa Simba Patrick Aussems amewatupia lawama wachezaji wake.
“Unajua wakati mwingine unaweza kupoteza pasi, control au hata kupiga mpira nje hilo sio tatizo, cha msingi ni mtazamo na akili za uwanjani zinabidi zitulie kama mchezaji muelevu lakini kwa bahati mbaya haikuwa hivyo kwetu niliwaambiwa wakati wa mapumziko kwamba kama hamtobadili mitazamo yenu uwanjani tutakutana na wakati mgumu lakini kipindi cha pili wakarudi vile vile wakidhani wanacheza na timu ya madaraja ya chini kwa hiyo itakuwa rahisi tu, nimesikitishwa na baadhi ya viwango vya wachezaji wangu hususani chipukizi” alisema kocha wa Simba Patrick Aussems
Ushindi huo sasa unawafanya timu ya Mashujaa FC kutoka Kigoma ifuzu kucheza hatua ya 32 bora ya michuano hiyo baada ya kuwaondoa Simba SC, hata hivyo hii sio mara ya kwanza kwa Simba SC kutolewa mapema katika michuano hii kwa timu zinazozaniwa kuwa vibonde , kwa msimu uliopita walitolewa kwa mikwaju ya penati na timu ya daraja la chini ya Green Warriors.