Fainali Kombe la EFL kuchezwa tarehe 24 Februari 2019
Chama cha soka nchini Uingereza kimetangaza kuwa tarehe rasmi ya kushuhudia kwa fainali ya Kombe la EFL ni siku ya Jumapili ya mwezi Februari 24 2019, wakati michezo ya kwanza itachezwa Januari 7 na kurudiana baada ya wiki mbili baadae.
Tottenham Hotspurs baada ya kufanikiwa kuwatoa majirani zao wa London klabu ya Arsenal kwa kuwafunga mabao 2-0 yaliofungwa na Son Heung-Min dakika ya 20 na Dele Ali dakika ya 59 wamepewa nafasi ya kucheza dhidi ya majirani zao wengine wa jiji la London kutoka Stamford Bridge klabu ya Chelsea.
Kwa upande wa nusu fainali ya pili Mabingwa watetezi wa Kombe hilo klabu ya Manchester City wao wanahusishwa kuwa na nafasi kubwa ya kutetea taji hilo kutokana na kucheza dhidi ya Burton Albion katika mchezo wa nusu fainali ambapo inaonekana kama vibonde Burton Albion ambao katika historia ya timu hiyo ndio mara yao ya kwanza kufikia hatua ya nusu fainali.
Burton Albion ambao wamewashitua wengi kutokana na uwezo wao hadi kufikia hatua hiyo, walifanikiwa kuingia nusu fainali kwa kuifunga Middlesbrough kwa bao 1-0 katika mchezo wa robo fainali, lakini wakitajwa kama timu ya kiwango cha chini zaidi katika hatua hiyo ya nne bora.