Hat-trick ya Jafari Kibaya imemuweka kwenye rekodi za Kaniki
Klabu ya Mtibwa Sugar imeandika historia mpya baada ya kucheza mchezo wake wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Northen Dynamo kutoka visiwa vya Ushelisheli na kufanikiwa kuifunga kwa mabao 4-0.
Ushindi wa Mtibwa Sugar katika mchezo huo wa mzunguuko wa kwanza unachagizwa na hat-trick ya Jafari Kibaya ambaye anacheza michuano hiyo kwa mara ya kwanza katika maisha yake na kufanikiwa kufunga hat-trick na kufikia rekodi ya Joseph Kaniki.
Jafari Kibaya alifunga mabao matatu dakika ya 12, 36 na 57 baadae dakika za nyongeza Riphat Khamis akafunga goli la nne la Mtibwa Sugar, baada ya kufunga hat-trick Kibaya anaifikia rekodi ya Joseph Kaniki ya ufungaji bora wa muda wote wa Mtibwa Sugar katika michuano hiyo akiwa na magoli matatu.
Tofauti ya Kibaya na Kaniki ni kuwa Kibaya amefunga magoli hayo katika mchezo mmoja na Kaniki katika michezo tofauti, Kibaya ana nafasi ya kubadili upepo kama ataweza kufunga goli jingine tena katika mchezo wa marudiano ambao Mtibwa atakuwa anahitaji sare ya aina yoyote au kupoteza kwa chini ya magoli 3 ili afuzu hatua inayofuata.