Paul Ince aziponda mbinu za Mourinho
Mkongwe wa soka wa Uingereza aliyewahi kukipiga katika klabu tofauti tofauti Paul Ince ambaye kwa sasa amekuwa akitumika kama mchambuzi wa soka kwa baadhi ya mechi, amefunguka na kuamua kumkosoa kocha wa Man United Jose Mourinho kuhusiana na mbinu zake.
Ince mwenye umri wa miaka 51 kwa sasa amewahi kuichezea Manchester United kwa takribani miaka sita kabla ya mwaka 1995 kuamua kuihama timu hiyo na kujiunga na Inter Milan ya Italia, ameungana na baadhi ya watu wanaopinga namna ya mfumo wa Manchester United anaoutaka Mourinho timu icheze.
Mkongwe huyo aliyekuwa akicheza nafasi ya kiungo amefika mbali zaidi na kumkosoa Mourinho kuwa haridhishwi na namna, Jose Mourinho anavyomchezesha Alex Sanchez.
“Mashabiki walizomea mwisho wa mchezo hivyo hawakuipenda Manchester United ilivyocheza “
“ Tunaizungumzia Manchester United na sio kuivunjia heshima Palace lakini kumuingiza Fellaini kabla ya Sanchez ni nini ulikuwa mpango wake ?
“ Kama Manchester United wanashindwa kufunga unamuingiza Fellaini…..”
Alisema kwa kuchukizwa Ince katika kipindi cha Match of the Day cha BBC.
Mechi hiyo iliisha kwa sare ya bila kufungana na Man United kushika nafasi ya saba, pointi 14 nyuma ya vinara wa ligi Man City