Simba SC kutoa taarifa rasmi leo muda ataokaa nje Kapombe
Beki wa wekundu wa Msimbazi Simba Shomari Kapombe bado yupo Cape Town Afrika Kusini akiendelea kupatiwa matibabu ya mguu wake ambao ulivunjika akiwa katika majukumu ya timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars kuelekea mchezo dhidi ya Lesotho.
Klabu ya Simba SC kupitia kwa afisa habari wao Haji Manara wametoa taarifa za awali kuhusiana na maendeleo ya mchezaji huyo ikielezwa kuwa tayari amefanyiwa upasuaji katika mguu wake na leo jioni ndio watatoa taarifa ya lini atarejea uwanjani au anakuwa nje ya uwanja kwa muda gani.
“Kapombe yupo Cape Town Afrika Kusini, tayari amefanyiwa oparesheni na leo tutapata taarifa rasmi kuwa tutamkosa kwa kipindi gani, nadhani leo jioni tutatoa taarifa rasmi baada ya kupata ripoti ya kitabibu wakati wachezaji wetu Juuko Murshind na Emmanuel Okwi wataingia usiku wa leo baada ya kumaliza majukumu yao kuitumikia Uganda” alisema Manara kuelekea mchezo wa Simba SC dhidi ya Mbabane Swallows mchezo wa klabu Bingwa Afrika.
Tukukumbushe tu Shomari Kapombe alivunjika mguuu dakika za mwisho wakati wa maandalizi kuelekea mchezo wa Taifa Stars dhidi ya Lesotho, mchezo wa kuwania tiketi ya kucheza michuano ya mataifa ya Afrika mwakani nchini Cameroon, hata hivyo Taifa Stars walipoteza mchezo huo kwa goli 1-0 wakimkosa Kapombe na nahodha wao Mbwana Samatta aliyekuwa anatumikia adhabu ya kadi mbili za njano.