Alichokisema Ronaldo baada ya Ozil kuondoka Real Madrid 2013
Mgeni njoo mwenyeji apone. Msemo huu wa waswahili hautumiki kila sehemu duniani. Mwaka 2012 Luka Modric alitua Real Madrid akitokea Tottenham. Ujio wake ulikuwa ni furaha kwa mashabiki wa Real Madrid na wachezaji, lakini si kwa mtu mmoja tu.
Huyu ni Mesut Ozil, ujio wa Modric haukuwa ni habari njema kwake kwani alifahamu dakika alizokuwa anacheza zitapungua.
Mwaka 2013 Mesut Ozil aliamua kuondoka kwenye timu hiyo baada ya kuitumikia kwa miaka mitatu akishinda kwa kombe moja tu.
Katika msimu wake wa mwisho nchini Hispania, aliweka rekodi ya kuwa na assist nyingi zaidi kuliko mchezaji mwingine yoyote kwenye ligi, lakini alijua kuwa nafasi yake ipo mashakani.
Simu ya Arsene Wenger iliingia katika simu yake, kocha huyo akiwa Arsenal akamuahidi kuwa endapo atajiunga na timu yake atamafanya kuwa mchezaji muhimu katika kikosi chake.
Mesut Ozil aliyaelewa maneno ya Arsenal Wenger, akakubali kusaini mkataba na washika bunduki hao.
Kama ilivyotarajiwa, kila shabiki wa Arsenal alishangilia ujio wa kiungo huyo bora duniani.
Ni mtu mmoja tu katika jiji la Madrid hakuwa na furaha na dili hilo kukamilika. Huyu ni Cristiano Ronaldo, hakufurahishwa kabisa
kutokana na faida alizokuwa akizipata kutoka kwa mchezaji huyo aliyekosa neno ubinafsi katika kamusi yake.
“ Kuuzwa kwa Ozil ni habari mbaya sana kwangu mimi. Alikuwa ni mchezaji bora aliyejua mienendo yangu mbele ya goli. Nina hasira kuhusu kuondoka kwa Ozil “ alisema Ronaldo baada ya kuondoka Ozil.
Ronaldo ambaye alikasirishwa na dili hilo, baadae alizoea kuondoka kwa Ozil na kurudi kucheza na nyavu kama kawaida.
Katika majira haya ya kiangazi Ronaldo alindoka Real Madrid baada ya miaka tisa nchini Hispania na kutua Juventus nchini Italia kwa ada ya pauni milioni 105.