Uganda waipa uchochoro Taifa Stars
Si ndoto tena, bali ni uhalisia kutokana na mipango. Kwa mara ya pili mfululizo timu ya Taifa ya Uganda wanafuzu michuano ya mataifa ya Africa.
Katika mechi ya jana ya kundi L, Uganda walikuwa wanahitaji pointi moja tu kufuzu michuano ya AFCON 2019 itakayofanyika nchini Cameroon, hawakupata sare, walipata zaidi ya pointi moja. Dakika ya 78 ya mchezo huo, mshambuliaji wa KCCA FC Patrick Kaddu aliifungia Uganda goli liliowapa ushindi wa 1-0 na kuwapeleka nchini Cameroon.
Wakati mwamuzi anajiandaa kupuliza filimbi ya mwisho, mashabiki wa Uganda walikuwa tayari wakishangalia, timu yao ikiwa imefuzu michuano ya AFCON kwa mara ya pili mfululizo.
Mpaka sasa Uganda wakiwa hawajapoteza mchezo wala kuruhusu kufungwa goli kwenye safari hii ya kufuzu AFCON 2019, wamekaa kwa raha mstarehe kileleni mwa kundi L wakiwa na pointi 13 huku wakiwa wamebakisha mechi moja tu ambayo watacheza na Tanzania mwezi Machi mwakani.
Kipigo cha Cape Verde jana katika ardhi ya Uganda kwenye uwanja wa Namboole, unawaweka Cape Verde katika hatihati ya kutopata nafasi ya kwenda Cameroon mwakani.
Endapo Tanzania itaifunga Lesotho leo huko Maseru, timu nyingine kutoka Afrika Mashariki itakuwa imepata tiketi ya kutua Cameroon mwaka 2019.
Tanzania haijawahi kufuzu michuano ya AFCON tangu mwaka 1980. Wakiwa nafasi ya pili mwa kundi L na pointi 5, wanahitaji kufikisha pointi 8 tu ili kupata nafasi ya kwenda kwenye michuano hiyo baada ya miaka 38.
Ushindi wa Uganda jana umeipa timu hiyo ya kocha Emmanuel Amunike njia nyeupe ya kwenda Cameroon