Man United wayarudia maajabu ya Camp Nou nchini Italy.
Mwamuzi kutoka Italy Pierluigi Collina Mei 26,1999 katika uwanja wa Camp Nou, jijini Barcelona nchini Spain alishuhuhudia moja ya maajabu katika maisha yake ya uamuzi wa mchezo wa mpira wa miguu.
Dakika ya 67 alimruhusu Sir Alex Ferguson afanye mabadiliko kwa kumtoa Jesper Blomqvist na kuruhusu Teddy Sheringham aingie uwanjani.
Baadae dakika ya 81 Collina aliombwa na Fergie tena kufanya mabadiliko ambapo safari hii Andy Cole ndiye aliyekwenda benchi na Ole Gunnar Solskjaer kuingia uwanjani.
Collina na wasaidizi wake pengine hakuna walichofahamu kuhusu mababiliko hayo, lakini Ferguson labda ndiye aliyekuwa na uhakika na kazi ya akili yake.
Man United wakiwa nyuma kwa goli moja dhidi ya Bayern Munich kwenye mchezo huu wa fainali klabu Bingwa Ulaya, dakika ziliendelea kuisha, Bayern wakisubiri filimbi ya mwisho ya Collina ili wachukue kombe lao.
United walipata kona huku mwamuzi wa akiba akionesha dakika 3 za nyongeza, Teddy Sheringham anarudisha goli katika dakika ya kwanza ya dakika za nyongeza baada Bayern kushindwa kuiokoa kona iliyopigwa na David Beckham.
United wakalazimisha kupata kona nyingine, Beckham akapiga tena kona na mpira ukatua kwa kichwa cha Sheringham ambaye aliupigia kuelekea golini, ukamkuta Ole Gunnar Solskjaer kwa haraka zaidi akauweka ndani ya wavu wa Oliver Khan.
Mechi inaisha kwa Man United kushinda 2-1 na kuwa mabingwa wa Ulaya. Ni moja ‘Comeback’ bora katika historia ya mpira wa miguu.
Wakati Muitalia Collina akishuhudia maajabu hayo, Waitalia wengine zaidi ya 35,000 wamekutana na maajabu ambayo alikutana nayo Collina mwaka 1999.
Jana haikuwa Camp Nou, ilikuwa ni katika uwanja wa Juventus, Allianz Stadium nchini Italy. Goli la Cristiano Ronaldo dhidi ya Man United dakika ya 65, lilidumu kwa muda mrefu na kuwapa matumaini mashabiki wa Juventus kuondoka na pointi 3 kwenye uwanja wao wa nyumbani kwenye mchezo wa kundi H klabu Bingwa Ulaya .
Safari hii alikuwa si Alex Ferguson, bali alikuwa ni Mreno Jose Mourinho aliyemuomba mwamuzi ili afanye mabadiliko kwa upande wa Man United. Juan Mata Garcia aliruhusiwa kuingia uwanjani dakika ya 79 akitoka Alexis Sanchez.
Zikiwa zimebaki dakika 5 mechi kuisha United wakapata free kick nje kidogo ya box la 18 la Juventus.
Kwa wanaomjua Juan Mata na eneo lile ambalo free kick ilipatikana, basi walishajua Man United wamesawazisha goli.
Na ndicho kilichotokea, Juan Mata anauweka mpira wavuni na kuisawazishia United dakika ya 86.
Mwaka 1999 United walivyosawazisha wakalazimisha kupata kona nyingine, safari hii baada ya free kick kuzaa matunda wakalazimisha kuipata nyingine, Ashley Young anapiga free kick na mabeki wa Juventus wanashindwa kuuondoa mpira mpaka kupelekea Leonardo Bonucci kujifunga.
Mechi inaisha kwa ushindi wa 2-1 kwa Man United ambao wanakuwa ni timu ya kwanza kuipa kipigo Juventus msimu huu.
Historia ya mwaka 1999 imeweza kujirudia tena jana katika Klabu Bingwa Ulaya.
Deja vu