Antonio Conte kuwapeleka Chelsea mahakamani
Meneja aliyeipa ubingwa Chelsea wa ligi ya England mwaka 2017 ,Antonio Conte anataka kuipeleka timu hiyo mahakamani akidai pesa kutokana timu hiyo kuvunja nae mkataba.
Muitalia huyo anataka kuipeleka timu hiyo mahakamani baada ya kuwakatalia kukaa nao meza moja kufanya mazungumzo.
Conte anawadai Chelsea Pauni milioni 20 ( Tsh Bilioni 60) ya mkataba wake ambao ulivunjwa ukiwa umebaki muda wa miezi 12 kuisha.
Bosi huyo wa zamani wa Juventus na Italy,anataka mshahara wake miezi 12 ambao ni pauni milioni 11.3 na pia anadai pauni milioni 8.7 kwa kuvunjiwa heshima yake.
Inaripotiwa kuwa Chelsea wanakataa kumlipa kocha huyo kutokana na tabia zake akiwa ndani ya klabu hiyo, zikiwamo jinsi alivyokuwa anamfanyia Diego Costa na kupelekea mchezaji huyo kuondoka mwezi Januari, kuchelewa kufika kwenye mikutano na waandishi wa habari, kushindwa kufika katika matukio ya wadhamini na pia sababu nyingine ni kocha huyo kushindwa kuegesha gari lake sehemu sahihi kwenye uwanja wa mazoezi Cobham.