Thierry Henry bado hajaona raha ya ukocha
Bado bundi la vipigo mfululizo visivyoisha linazidi kuiandama klabu ya AS Monaco ya Ufaransa chini ya kocha wake mpya Thierry Henry ambaye toka amejiunga na klabu hiyo mwaka huu October 13 2018 hajapata ushindi wowote.
Kwa lugha rahisi unaweza kusema kuwa kocha wa AS Monaco Thierry Henry hadi leo hii hajaona raha ya ushindi toka awe kocha wa AS Monaco, Henry amekuwa akiandamwa na vipigo na sare pamoja na kuletwa October 13 2018 aje ainusuru klabu hiyo ambayo kwa sasa ipo katika hali mbaya ki-uwezo uwanjani.
Baada ya AS Monaco kufungwa leo kwa magoli 4-0 dhidi ya Club Brugge ya Ubelgiji katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya inakuwa imeshindwa kupata ushindi katika mechi zake za mashindano yote 15 mfululizo msimu huu, ikipoteza kwa jumla ya michezo 10 kati ya 15 na kutoka sare michezo mitano.
Kipigo hicho sasa kinaiweka Monaco katika hali mbaya katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu, kwani kuwa kinawafanya waage mashindano hayo wakiwa na michezo miwili mkononi, kwani hata akishinda michezo yote miwili hawezi kufikia alama 9 walizonazo Borussia Dortmumd na Atletico Madrid.
Tukukumbushe tu magoli manne ya Club Brugge dhidi ya AS Monaco yamefungwa na Hans Vanaken dakika ya 12 na 17 kwa penati, Wesley Moraes dakika ya 24 na Ruud Vormer dakika ya 85, Monaco msimu huu amekumbwa na wakati mgumu kwani hata Ligi Kuu Ufaransa ameshinda mechi moja kati ya 10 na yupo nafasi ya pili kutoka mwisho katika Ligi yenye timu 20.