Leicester City wampa zawadi mmiliki wao
Cardiff City Stadium ni uwanja ambao mara zote timu ya ugenini hupokelewa kiuadui. Hali haikuwa hivyo siku ya jana. Wachezaji wa Leicester City wakati wanaingia uwanjani kupasha misuli kabla ya mechi, huku wakivalia T-shirt ikiwa na picha ya Vichai Srivaddhanaprabha kwa mbele, walishangiliwa sana na mashabiki wa Cardiff.
Nyuma ya T-shirts zao ziliandikwa ‘ Khun Vichai. You Will Be Forever In Our Hearts,’ yaani ‘ Khun Vichai. Milele utakuwa katika mioyo yetu.
Kabla ya mchezo kuanza,watu wote uwanjani walisimama na kukaa kimya kwa dakika moja, wakiomboleza kifo cha bilionea huyo kilichotokea jumamosi iliyopita kwa ajali ya helikopta.
Wakati timu zinaingia uwanjani , Banner kubwa yenye bendera ya Thailand na beji za Leicester City na Cardiff, ikiwa na maandishi ya ‘ RIP Vichai ‘ ilipita katika vichwa vya mashabiki wa Cardiff City kuelekea kwa mashabiki wa Leicester City.
Leicester City wakaibuka na ushindi wa 1-0 katika mechi hiyo ya majonzi, ikiwa ni mechi yao ya kwanza tangu mmiliki wao huyo kutoka Thailand afariki.
Demarai Gray ndiye aliyefunga goli la ushindi muda mchache baada ya kutoka mapumziko na timu zima ilishangilia kwa hisia mbele ya mashabiki wao waliosafiri kuja Wales.
Winga huyo alipewa kadi ya njano kwa kuvua jezi yake na kuonesha maandishi yalioyoandikwa kwa nguo ya ndani “ for Kun Vichai “ , akiwa amelitoa goli hilo kwa Vichai.
Ushindi huo wa 1-0 ugenini, unawafanya ‘The Foxes’ wawe nafasi ya 10 wakiwa na pointi 16 huku Cardiff wakiendelea kubakia katika nafasi ya kushuka daraja,wapo nafasi ya 18 wakiwa na pointi 5.
Baada mchezo kumalizika, kikosi cha Leicester City kilienda katika uwanja wa ndege wa Cardiff, kuchukua ndege kuwapeleka Bangkok ili waweze kuhudhuria shughuli za mazishi zilizoanza tangu jumamosi.