Samatta kafunguka kuelekea mchezo wao wa Kesho
Jumamosi hii klabu ya KRC Genk itacheza mchezo wa Ligi Kuu Ubelgji (Jupiter Pro League) dhidi ya Club Brugge ambao watakuwa ugenini kuikabili Genk ambao ndio vinara wa Ligi Kuu kwa sasa wakifuatiwa na Club Brugge.
Mchezo wa Genk na Brugge unazidi kuleta hamasa kubwa kwa mashabiki wa soka katika mji wa Genk kutokana na timu yao kufanya vizuri sana, hususani katika michezo ya Ligi Kuu na michuano ya Europa League.
Baadhi ya mitandao ya habari za michezo nchini Ubelgiji imeripoti kuwa mchezo huo ambao una nafasi ya kuamua Genk aendelee kuongoza Ligi au Club Brugge arudi kileleni, unatajwa kuwa tiketi za mashabiki za kuingia uwanja wa Luminus Arena zimemalizika tayari.
Kuelekea mchezo huo mtanzania Mbwana Samatta anayeichezea KRC Genk ambaye pia ni mshambuliaji tegemeo wa timu hiyo akiwa kinara wa wafungaji kwa kuwa na magoli 10 akifuatiwa na Ivan Santini wa Anderletch, Samatta amefunguka kuelekea mchezo huo.
“Kiukweli kesho utakuwa ni mchezo wenye changamoto sana na hatutarajii kuwa utakuwa mchezo rahisi kwetu lakini kama tutashinda mchezo wa kesho maana tutakuwa tunaongoza kwa tofauti ya point sita dhidi yao ninaamini wachezaji wote wapo sawa na tunataka pointi tatu” alisema Samatta alipohojiwa na Genk TV
Samatta pia aliongezea kwa kueleza kuwa sababu zilizokuwa zinamfanya wakati mwingine ashindwe kufunga “Kwenye maisha sio kila wakati utakuwa ni mzuri tu, kuna wakati mambo yatakuwa vizuri na kuna wakati yatayumba hayawezi kuwa mazuri, ni ngumu hivyo ninatakiwa kukubaliana na kuielewa hiyo hali, tiketi kuuzwa zote ina maana kuwa tutakuwa na mashabiki wengi kesho na itatusaidia kumshinda mpinzani”
KRC Genk kesho watacheza na Club Brugge katika mchezo wao wa 14 wa Ligi Kuu Ubelgiji (Jupiter Pro League) msimu huu, Genk wakiongoza kwa kuwa na alama 33 wakati Brugge wakishika nafasi ya pili kwa kuwa na alama 30, hata hivyo Club Brugge hawana kumbukumbu nzuri katika uwanja huo, kwani mchezo wao dhidi ya Genk msimu uliopita walipoteza kwa magoli 2-0 October 25 2017 katika mchezo wa Ligi Kuu.