De Bruyne apeleka majanga tena kwa Guardiola.
Kevin De Bruyne anafanyiwa uchunguzi na madaktari wa Man City baada kuonekana kuumia katika goti lake la kushoto katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Fulham jana kwenye raundi ya nne ya Carabao Cup.
Kocha wa Man City Pep Guardiola amekiri kuwa na wasiwasi kuhusu kuumia kwa mchezaji huyo ambapo alitolewa uwanjani kunako dakika ya 86 kwenye mchezo huo uliopigwa Etihad Stadium.
Akihojiwa na Sky Sports baada ya mechi kumalizika Guardiola alisema “ (Tatizo) linaangaliwa na daktari. Kwa sasa sijui kama hakuna kitu au kuna kitu kikubwa “
De Bruyne hivi karibuni amerejea dimbani akitokea kuuguza majeraha ya goti lake la kulia yaliyomuweka nje ya uwanja kwa muda wa miezi miwili.
Mbelgiji huyo alianguka chini baada ya kujaribu kuuchukua mpira kutoka kwa beki wa Fulham Fosu-Mensah katika kona ya uwanja, na Mensah kumuangukia kwenye mguu wake wa kushoto.
KDB alionekana mwenye majonzi wakati akitoka uwanjani na kuelekea moja kwa moja vyumbani akiwa na timu ya matabibu.
Brahim Diaz alifunga goli zote mbili na kuwapeleka na mabingwa watetezi wa Carabao Cup robo fainali ambapo watakutana na mshindi kati ya mechi ya Leicester City na Southampton.