Leicester City waukataa usafiri wa ndege
Baada ya kufiwa na mmiliki wao Vichai Srivaddhanaprabha, Leicester City waliahirisha mchezo wao Carabao Cup wa jana jumanne dhidi ya Southampton na ilitazamiwa mchezo wao wa Jumamosi Cardiff huenda ungeahirishwa pia.
Klabu hiyo jana ilitangaza jana kuwa mchezo huo wa ligi kuu dhidi ya Cardiff itachezwa kama ilivyopangwa huku wakiendelea na maombolezo.
Awali ilipangwa wasafiri mpaka Wales kwa usafiri wa ndege, lakini wamebadilisha usafiri huo na sasa watakwenda kwa usafiri wa basi.
Imeelezwa kuwa wameamua hivyo baada ya kukubaliana kwamba kusafiri kwa ndege itaonekana kutojali mazingira ya kifo cha Vichai.
Maandalizi yalishafanywa kuondoka kwa ndege, kama ilivyo kawaida katika safari za mbali kwenye mechi za ugenini, lakini badala yake timu hiyo itasafiri kwa basi kwa muda wa saa tatu siku ya ijumaa.
Viongozi mbalimbali wamekubali maamuzi hayo ambayo yameungwa mkono na kocha Claude Puel na wachezaji wote na benchi la ufundi.