“Sikupewa heshima niliyokuwa napewa kama mwanzo“-Ronaldo
Huku timu ya Real Madrid ikiwa katika kiwango kibovu kwa sasa, mchezaji Cristiano Ronaldo amemrushia lawama Rais wa klabu hiyo Florentino Perez kuwa ndiye sababu kubwa ya yeye kuondoka na kujiunga na klabu ya Juventus ya nchini Italia.
Baada ya miaka tisa ya kuitumikia klabu hiyo kapteni huyo wa timu ya taifa ya Ureno aliondoka na kujiunga na kibibi kizee cha Turin.
Katika mahojiano yake na France football alikaririwa akisema “Nilihisi ndani ya klabu hasa kwa upande wa Rais sikuwa na mashiko tena kama hapo mwanzo. Miaka minne ama mitano ya kwanza nilikuwa nikihisi uwepo wangu mimi kama Cristiano Ronaldo
Ila taratibu ulianza kupotea na kwa kumuangalia Rais nilihisi kutohitajika kama mwanzo.”
Kwa miaka 9 aliyokaa Madrid ameshinda jumla ya mataji 16 na kufunga magoli 450.
“Habari zilipoanza enea kuwa nataka kuondoka nilipata hisia kama Rais hatonizuia kuondoka” amesema Ronaldo
Mreno huyo ndiye mfungaji bora wa muda wote kwa klabu ya Madrid akiwa ameweza pata mafanikio binafsi kwa kuchukua Baloon d’Or nne katika tano alizonazo.
Tokea kuondoka kwake, klabu ya Madrid imekuwa katika kiwango kibovu na wikiendi iliyopita wamepata kipigo cha magoli 5 – 1 dhidi ya Barcelona .
“Kuondoka kwangu hakukuja kama matokeo ya kuondoka kwa kocha Zinedine Zidane bali lile lilikuwa ni moja ya jambo lililonipa uhakika wa hali ilivyokuwa ikiendelea klabuni hivyo halikunizuia “
Baada ya kuondoka kwa Zidane, Madrid walimchukua kocha wa timu ya taifa ya Hispania Juletn Lopetegui ambaye ametimuliwa jana baada ya kuwa na matokeo mabovu.