Julen Lopetegui atimuliwa Santiago Bernabeu
Jipu likishaiva, ni kutumbuliwa tu ili kutoa usaa uliondani. Julen Lopetegui katika klabu ya Real Madrid ni jibu ambalo lilishaiva na muda wake wa kutumbuliwa ulishafika, na kama lingechelewa kutumbuliwa basi madhara yangekuwa makubwa.
Real Madrid wamemfuta kibarua kocha huyo kutokana na kuwa na matokeo mabovu tangu aichukue timu hiyo majira ya kiangazi mwaka huu, na nafasi yake inachukuliwa na kocha wa kikosi B Santiago Solari ambaye ana kaimu nafasi hiyo kwa muda.
Timu hiyo inataka kumuacha Solari katika nafasi hiyo mpaka mwezi ujao katika mapumziko ya mechi za kimataifa na baada ya hapo watamtangaza kocha ambaye atapewa mkataba wa kudumu.
Fiorentina Perez anataka kocha wa zamani Antonio Conte kuja kuchukua nafasi hiyo lakini Muitalia huyo anahitaji mkataba wa miaka miwili na nusu na kuwa na wasaidizi watano, hivyo inaweza kumpa ugumu Perez kumpa kazi hiyo na kwenda kwa chaguo lingine ambalo ni kocha wa timu ya Taifa ya Belgium Roberto Martinez.
Kipigo cha 5-1 kutoka kwa Barcelona jumapili iliyopita, ilikuwa ni kama kugongelea msumari katika kidonda cha Julen Lopetegui.
Lopetegui,52, alitangazwa kuwa kocha wa Real Madrid Juni 14 mwaka huu. Wakati huo alikuwa kocha wa timu ya Taifa ya Spain, ambapo akatimuliwa kazi hiyo muda mchache baada ya kutangazwa kuwa kocha wa Real Madrid.
Akiwa na Real Madrid ameweza kushinda mechi 6 tu kati ya 14 alizoiongoza timu hiyo.
Mhispania huyo anaondoka akiicha Real Madrid ikiwa nafasi ya 9 katika msimamo wa La Liga wakiwa na Pointi 14, Pointi 7 nyuma ya vinara Barcelona.