Barcelona yamuweka pabaya Julien Lopetegui
El Clasico ya kwanza bila Cristiano Ronaldo na Lionel Messi tangu mwaka 2007.
Hii ilikuwa ni mechi watu wa soka walikuwa wakiingoja kuona ni nani atakuwa nyota wa mchezo, Luis Suarez anawapa majibu hayo katika dimba la Camp Nou, akifunga goli tatu na kuondoka na mpira kwenye ushindi wa 5-1 nyumbani.
Philippe Coutinho ndiye aliyekuwa wa kwanza kufungua ukurasa wa magoli katika dakika ya 11 ya mchezo akiunganisha pasi nzuri kutoka kwa beki wa kushoto Jordi Alba.
Dakika ya 30 Luis Suarez akaiweka Barcelona mbele kwa goli mbili kwa kufunga kupitia mkwaju wa penati aliopata baada ya kuchezewa rafu na Raphael Varane ndani ya Box.
Marcelo anafunga katika mechi ya tatu mfululizo ya Real Madrid kunako dakika ya 50 na kurudisha matumaini ya Julen Lopetegui kurejea mchezoni.
Wakati Real Madrid wakiwa wamerudi kwenye hali ya mchezo , Luis Suarez anawakatisha tamaa kwa kufunga kichwa kizuri dakika ya 75 akimalizia krosi Sergi Roberto.
Luis Suarez anajihakikishia kuondoka na mpira kwa kufunga goli la tatu dakika ya 83 na kuwa mchezaji wa kwanza kufunga hat trick katika El Clasico tangu Lionel Messi afanye hivyo Machi 2014.
Arturo Vidal ambaye alishawahi kusema hawapendi Real Madrid, anafunga ubao wa magoli wa Barca kwa kuweka kambani goli la 5, na hili ndio goli lake la kwanza tangu ajiunge na wacatalunya hao majira ya kiangazi mwaka huu.
Shukurani za mashabiki wa Real Madrid zinaenda kwa Lionel Messi ambaye ameshindwa kucheza mechi hii ya leo kutokana na kuwa ameumia mkono, hivyo pengine angekuwepo wangepokea goli nyingi zaidi.
Kuachana na mashabiki wa Real Madrid, Luis Suarez ni mmojawapo wanaoshukuru kutokuwepo kwa Lionel Messi, ambapo kumefanya aondoke na mpira, ikiwa ni zawadi ya mwanae wa kiume, Lauti aliyezaliwa katika juma hili.
Ushindi huu unawafanya Barcelona waendelee kukaa kileleni mwa La Liga wakiwa na pointi 21, wakiwapita Real Madrid pointi 7.
Real Madrid hii ni mechi ya 4 kupoteza katika La Liga msimu huu, na sasa wapo nafasi ya 9 wakiwa na pointi 14.
Hii ni ishara tosha kwa kocha Julen Lopetegui muda wake wa kukaa Bernabeu umefika kikomo licha ya kuwa ametua majira ya kiangazi mwaka huu.