Vijana wa mapango ya Thailand kutazama mechi ya Manchester United Vs Everton Old Trafford
Watoto 12 waliookolewa toka katika mapango nchini Thailand Julai mwaka huu watahudhuria mechi ya Manchester United dhidi ya Everton katika dimba la Old Trafford leo jumapili.
Taarifa ya watoto hawa wenye miaka 11 hadi 16 ambao ni wachezaji wa timu ya watoto ya Wild Boar kunasa ndani ya pango lililojaa maji pamoja na kocha wao ilienea dunia nzima na baadae wakafanikiwa kuokolea wote.
Baada ya kuokolewa walipata mualiko wa kwenda Old Trafford toka kwa makamu mwenyekiti mtendaji wa Man United Ed Woodward.
Jana wametua Old Trafford na kukutana na kocha Jose Mourinho na nyota wengine wa timu hiyo wakiwamo Paul Pogba, Ashley Young, Martial na wengine na watapata nafasi ya kutembea katika viunga mbali mbali vya uwanja kabla ya mechi.
Mapema mwezi huu walipata nafasi ya kwenda nchini Argentina ambapo walicheza mechi za kirafiki katika uwanja wa Monumental Stadium uwanja uliotumiwa kwa fainali za kombe la dunia mwaka 1978.
Vile vile mwanzoni mwa mwezi huu walialikwa katika kipindi cha televisheni cha Ellen DeGeners cha Marekani.
Katika show hiyo, vijana hawa walipewa Surprise ya kuonana na nyota wa timu ya LA Galaxy Zlatan Ibrahimovic punde baada ya kumtaja kuwa ni ‘Role Model’ wao , na ndipo Zlatan alipopanda jukwaani kuketi nao na kwa mara ya kwanza alikubali kushindwa baada ya kusema yeye ni jasiri ila watoto hawa ni majasiri kumzidi na kwake ni timu bora duniani.
Mchezaji wa Manchester City Kyle Walker aliomba kuwatumia jezi ya timu ya taifa ya England watoto hao baada ya tukio hilo kutokea kufuatia kuguswa hasa na mtoto aliyekuwa amevalia fulana ya timu hiyo ya taifa.