HIZI NDIO TIMU SABA AMBAZO YAYA TOURE ANAWEZA KUUNGANA NAZO
Baada ya mchezaji wa zamani wa Manchester City Yaya Toure kuvunja mkataba wa kuitumikia timu ya Olympiakos ya Ugiriki akiwa amedumu nayo kwa kipindi cha miezi mitatu, ameamua kurudi Uingereza wakati huu akitafuta timu mpya ya kujiunga nayo.
Toure amerejea Uingereza kwa ajili ya kutafuta timu ya muda ya kufanya nayo mazoezi akiwa anasubiria ofa za kujiunga nazo licha ya tayari kuhusishwa kukataa ofa za kwenda kucheza Ligi Kuu ya nchini Marekani MLS na kwenda kucheza Ligi Kuu ya China.
Hata hivyo Toure amethibitisha kuwa anania ya kurudi kucheza soka Uingereza ambapo alikuwa akicheza Manchester City kwa miaka nane toka alipojiunga mwaka 2010 akitokea Barcelona na kudumu hadi 2018, hata hivyo bado hajaweka wazi atajiunga na timu gani.
Kwa mujibu wa moja kati ya mtandao wa habari za michezo Ulaya, Toure anahusishwa kujiunga na moja kati ya klabu hizi saba ambazo ni West Ham United, Fulham, Fenerhbace, Shaghai SIPG, Celtic, New York City na Melbourne City.