Mathare yawasajili wanne
Klabu ya Mathare United imewasajili wachezaji wanne wapya kabla ya msimu wa 2018-19 ambao utaanza siku ya Jumamosi.
Wanne hao ni pamoja na mshambulizi Kevin Kimani ambaye anarejea Mathare, klabu aliyoigura mwaka wa 2012. Kimani ametokea timu ya Sofapaka.
Wengine ni viungo wa kati James Kinyanjui ambaye ametokea klabu iliyoshushwa daraja ya Thika United na Arnold Onyango ambaye ametokea Shuleni.
Wa nne ni beki wa kushoto Samuel Semo ambaye aliwahi kuichezea timu ya wachezaji wachanga ya Mathare United.
“Nina furaha kurejea Mathare United. Hii ni timu iliyonikuza kama mchezaji na nitafanya bidii ili niweze kuisaidia timu,” alisema Kimani.
Kwa upande wake, Kinyanjui ambaye bado ni kiungo mchanga alisema anataka kujikuza kimchezo.
“Mathare ni timu ambayo ina historia ya kuwakuza wachezaji wachanga. Nina imani kuwa mchezo wangu utaimarika hapa,” alisema kwenye mahojiano.