“ Sitorudia kosa tena “ – Jurgen Klopp
Kocha wa klabu ya Liverpool Jurgen Klopp ameeleza kuwa hajutii kosa la kushangilia kwa kuingia uwanjani ambalo limefanya apigwe faini ya pauni 8000 sawa na shilingi milioni 23 za Tanzania.
Klopp alikimbia na kuingia uwanjani baada ya Divock Origi kuifungia Liverpool bao la ushindi dhidi ya Everton katika sekunde za mwisho za mchezo jumapili iliyopita Disemba 3 katika dimba la Anfield.
Chama cha soka cha England FA kilitangaza kumshitaki kwa kosa hilo na kumpa muda mpaka kesho alhamisi saa 12 jioni awe ameshajibu, lakini kocha huyo aliamua kukubali kosa hilo jumatatu usiku na kuahidi kuwa hatalifanya tena.
“ Faini ipo kwa ajili ya kukuweka makini na kufanya usifanye kosa tena. Kwa sasa ninajua, sitofanya tena “ Alisema Jurgen Klopp.
Kocha wa Everton Marco Silva ambaye aliombwa msamaha na Klopp baada ya mchezo huo jana jumanne alitoa jibu ambalo liliwashangaza wengi ,akisema “ Ukiniuliza mimi, ninafikiri hakutakiwa kupigwa faini, lakini FA wameamua (kutumia) sheria. Kwa hakika, kwa wakati ule, meneja hawezi kufikiri kuhusu faini. Ni muda wa kushangilia . “