Jose Mourinho aifuta ahadi yake
Mipango si matumizi, huu ni moja ya msemo maarufu kwa watumiaji wa lugha ya kiswahili.
Novemba 23 mwaka huu kocha wa Man United Jose Mourinho alisema kuwa anaamini timu yake itakuwa katika nne bora ya ligi kuu nchini England mwishoni mwa mwezi wa 12 mwaka huu.
Sasa kocha huyo kwa kinywa chake cha Novemba 23, ameamua kuifuta ahadi hiyo aliyoiweka, huku akisema kuwa Man United msimu huu kumaliza katika nafasi ya kucheza klabu bingwa Ulaya itakuwa ni miujiza.
United ambao walimaliza nafasi ya pili msimu jana, kwa sasa wapo nafasi ya saba katika ligi , wakiwa pointi nane nyuma ya timu ya nafasi ya nne Arsenal ambao wanakutana nao kesho kwenye mchezo wa ligi utakaopigwa Old Trafford.
“ Wiki iliyopita kabla ya kucheza na Crystal Palace nilisema matumaini na malengo yangu mwishoni mwa mwezi Disemba tutakuwa katika nafasi hiyo (nne bora).
Malengo yanabadilika lakini subiri tujaribu kupunguza umbali kwa kadri tunaweza na kuwa karibu zaidi ya nafasi hizo . “ Jose Mourinho aliiambia Televisheni ya Brazil Rede TV baada ya sare ya 2-2 dhidi ya Southampton jumamosi iliyopita.
Man United ambao wamefuzu hatua ya mtoano katika michuano ya klabu bingwa Ulaya wiki iliyopita, hawajashinda katika michezo mitatu ya mwisho ya ligi , wakipoteza mmoja na kutoka sare mara mbili.