Luka Modric avunja utawala wa Messi na Ronaldo
Huu ni mwisho wa ufalme wa Lionel Messi na Cristiano Ronaldo ?!
Usiku wa jana katika jiji la Paris historia mpya katika ulimwengu wa soka imeandikwa. Kwa muda wa miaka 10 ni watu wawili tu duniani ndio walikuwa wametawala tuzo ya Ballon d’Or, Cristiano Ronaldo.
Luka Modric ndiye aliyevunja utawala wa wachezaji hao wawili kwa kubeba tuzo ya Ballon d’Or mwaka 2018 akipata pointi 753 katika kura alizopigiwa, huku Cristiano Ronaldo akiachwa mbali, akiwa nafasi ya pili amepata pointi 476 na mshindi wa tatu akiwa bingwa wa kombe la Dunia 2018 Antoine Griezmann na namba 4 akiwa Kylian Mbappe.
Mashabiki wa soka wengi wameduwaa kwa Lionel Messi kushika nafasi ya tano kwenye kinyang’anyiro hicho na hii ni mara ya kwanza Messi kuwepo nje ya tatu bora katika tuzo hiyo tangu mwaka 2006.
Mwaka 2018 umekuwa ni mwaka mzuri kwa Luka Modric, akichukua ubingwa wa Klabu bingwa Ulaya na Real Madrid, michuano ya kombe la Dunia akaifikisha Croatia katika fainali.
Tuzo zingine alizobeba mchezaji huyo ni mchezaji bora wa UEFA, mchezaji bora wa kiume wa FIFA na mchezaji bora wa michuano wa kombe la Dunia.