Mbwana Samatta kashuhudia rekodi ya Genk ikivunjwa
Klabu ya KRC Genk ya nchini Ubelgiji imeendelea na michezo yake ya Ligi Kuu Ubelgiji msimu wa 2018/2019 kwa kuwakaribisha klabu ya Cercle Brugge katika uwanja wao wa nyumbani wa Luminus kucheza mchezo wa 16 wa Ligi Kuu nchini Ubelgiji maarufu kama Jupiler Pro League.
Mchezo huo uliyochezwa Luminus Arena jana Novemba 24, Mbwana Samatta alikuwa sehemu ya kikosi cha KRC Genk kilichoongoza safu ya ushambuliaji ya timu hiyo wakiwa katika uwanja wao wa nyumbani wenye uwezo wa kuingia mashabiki 23718.
Genk wakiwa nyumbani wanaruhusu kupoteza mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu Ubelgiji msimu huu, kwa kufungwa magoli 2-1, Cercle Brugge wakipata magoli kwa Joseph Aidoo wa KRC Genk kujifunga dakika ya 26 na Serge Gakpe kufunga goli la mwisho la Brugge lililoipa ushindi timu hiyo dakika ya 35 huku goli la Trossard dakika ya 90 likiwafuta machozi mashabiki wa Genk waliojitokeza uwanjani hapo.
Matokeo hayo yanaifanya Genk kuvunja rekodi yao ya kucheza michezo 15 ya Ligi Kuu Ubelgiji bila kupoteza msimu huu lakini ndio inakuwa timu ya mwisho kupoteza mchezo msimu huu katika timu zote 16 zinazoshiriki Ligi Kuu Ubelgiji msimu huu na inabaki kuwa timu pekee iliyofungwa mchezo mmoja Ligi hiyo msimu huu.
KRC Genk baada ya kupoteza mchezo huo wanaendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu kama kawaida wakiwa na alama 35 wakifuatiwa na Club Brugge waliopo nafasi ya pili wakiwa na alama 31 tofauti ya alama nne na Genk, Kwa upande wa Cercle Brugge waliovunja rekodi ya Genk wao wametimiza jumla ya alama 22 wakipanda hadi nafasi ya nane.