Fainali ya Superclasico yaahirishwa kwa vurugu
Mechi ya marudiano ya fainali ya Copa Libertadores inayowakutanisha mahasimu wawili River Plate na Boca Junior iliyokuwa ichezwe usiku wa jana jumamosi iliahirishwa kutokana na basi lililokuwa limebeba kikosi cha Boca Junior kupigwa na mashabiki wa River Plate na kusababisha kuumia kwa wachezaji
Chupa zilirushwa na wenyeji River Plate, na kuvunja vioo vya basi la Boca Junior likiwa linaingia katika uwanja wa El Monumental na kusababisha kuumia kwa baadhi ya wachezaji ambao waliwahishwa hospitali
Pablo Perez na Gonzalo Lamardo ndio wachezaji wa Boca Juniors walioumia na kupelekwa hospitali.
Baada ya vurugu hizo kutokea polisi walibidi kuachia bomu la machozi ili kuwasambaratisha mashabiki hao.
Hata hivyo, bomu hilo la machozi liliwaathiri wachezaji wa Boca Junior wakiwa kwenye basi. Mchezaji wa zamani wa Man United Carlos Tevez akiwa mmojawapo.
Muargentina huyo alioneshwa kwenye Televisheni akiwa anasaidiwa kuingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.
Kwa mujibu wa ripoti za nchini Argentina, wachezaji wenzake wa Boca Juniors walikuwa wanatapika katika vyumba vya kubadilishia nguo kutokana na kuathiriwa na bomu hilo.
Muda wa mechi hiyo kuanza ulisogezwa mbele lakini baadae ikatangazwa kuwa haitachezwa tena jumamosi, itachezwa siku ya jumapili Novemba 25 saa 11:00 jioni kwa saa za Argentina.
Mechi ya kwanza iliyochezwa majuma mawili nyuma, iliisha kwa sare ya 2-2.