Mchezaji wa Wales aomba ndege ya Gareth Bale
Mei 3 mwaka huu Floyd Mayweather aliamka asubuhi nyumbani kwake nchini Marekani akiwa hajisikii vizuri, akaita marubani wake na kupanda ndege yake na kwenda zake Singapore kuweka akili yake sawa.
Kesho yake hakubaki tena Singapore,alikwea pipa lake na kutua mjini Bali, Indonesia kula maisha.
Si kila mtu anayeweza kufanya hayo mabalaa ya Floyd Mayweather.
Beki wa klabu ya Reading Chris Gunter kesho jumanne atacheza mechi yake ya 93 katika timu ya taifa ya Wales na kuwa mchezaji aliyecheza mechi nyingi kuliko mwingine yoyote katika timu hiyo, anavunja rekodi ya kipa Neville Southall ambaye amecheza mechi 92.
Gunter,29, anataka familia yake iwepo uwanjani kushuhudia akivunja rekodi hiyo katika mchezo huo wa ugenini dhidi ya Albania ambao ni wa kirafiki.
Gunter amesema atajaribu kuazima ndege ya mchezaji mwenzake wa Wales, Gareth Bale ili aweze kuisafirisha familia yake yote mpaka nchini Albania kumshuhudia akicheza mechi hiyo ambayo itakuwa ni ya kihistora kwake.
Gareth Bale anayekipiga katika klabu ya Real Madrid anamiliki ndege ya Cessna Citation XL Plus yenye thamani ya pauni milioni 9.35 (sawa na Tsh Bilioni 27.6).
“ Nitamuuliza Gaz ( Gareth Bale) kama nitaweza kumuazima ndege yake “ Alisema Gunter
“ Si sehemu rahisi kufikika. Lakini ninafikiri kama mashabiki wa Wales wanaweza kufika nina hakika nitatafuta njia “
Kocha wa timu ya taifa ya Wales Ryan Giggs amesema Gunter ataanza katika mechi hiyo, huku Gunter akisema kuwa Albania ni sehemu nzuri ya kuvunja rekodi ya Southall.