Kutoka kwa Steph Curry mpaka kwa Eden Hazard
Mwaka 2016 katika fainali ya ligi ya mpira wa kikapu nchini Marekani NBA Golden State Warriors walikuwa wanahitaji kushinda mechi 1 tu ili kuwa mabingwa wa ligi hiyo, hii ni baada ya kuwa wanaongoza kwa 3-1 katika fainali hiyo.
Steph Curry na kocha wake hawakuamini kilichotokea, Cavs walifanya ‘Comeback’ ya kihistoria katika michezo, walishinda mechi tatu mfululizo na kuibuka mabingwa wa NBA msimu huo kwa kushinda mechi 4-3 .
Mdogo wake Eden Hazard, Thorgan Hazard anafunga goli mbili na kuifanya Belgium kuwa mbele kwa goli 2-0 katika dakika ya 17 dhidi ya Switzerland kwenye mchezo wa Kundi 2 katika League A kwenye UEFA Nations League jana nchi Switzerland.
Hivyo, Switzerland wakawa wanahitaji kufunga magoli manne ili kufuzu hatua ya fainali ya michuano hiyo.
Dakika ya 26 Ricardo Rodriguez akawapa matumaini Switzerland kwa kufunga goli kupitia mkwaju wa penati, kabla ya Haris Seferovic kusawazisha dakika ya 31.
Seferovic akawapa matumaini mashabiki wa Switzerland kwa kufunga goli la uongozi dakika moja kabla ya mapumziko.
Kama ilivyokuwa kwa Steph Curry na kocha wake Steve Kerr mwaka 2016, safari hii ni Eden Hazard na kocha wake Roberto Martinez hawakuamini kuisikia filimbi ya mwisho ya mwamuzi kutoka Italy Daniele Orsato huku ubao wa magoli ukisoma Switzerland 5-2 Belgium, Haris Seferovic akiondoka na mpira baada ya kufunga Hat Trick.
Switzeland sasa itacheza nusu fainali ya UEFA Nations League Juni 2019 pamoja na timu za Portugal, England na France au Netherlands