Ndoto ya Tanzania kwenda Cameroon yafifia mjini Maseru
Mwaka 1980 Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ndiye aliyekuwa ikuluĀ . Nchi ya Tanzania ilikuwa ikiongozwa kwa mfumo wa chama kimoja. Rais wa sasa wa Tanzania Mheshimiwa Dkt.John Pombe Magufuli alikuwa na umri wa miaka 21, alikuwa hata hajaanza kufundisha katika shule ya sekondari ya Sengerema.
1980 ndio ilikuwa mara ya mwisho Tanzania kucheza katika michuano AFCON, walikwenda kwenye michuano hiyo ikiwa imepita miezi 9 tangu Mwalimu J.K.Nyerere kumshinda Iddi Amin dada kwenye vita kati ya Tanzania na Uganda.
Mwaka huo Tanzania wanashiriki michuano ya AFCON, kocha wa sasa Tanzania Mnigeria Emmanuel Amunike alikuwa na umri wa miaka 10.
Leo ikiwa imepita miaka 38, kocha huyo na kikosi chake wameshuka dimbani na timu yake katika uwanja wa Setsoto mjini Maseru kucheza na Lesotho ugenini kutafuta nafasi ya kwenda AFCON.
Taifa Stars ilihitaji kupata pointi tatu tu ili kufuzu michuano hiyo. Matokeo yamekuwa tofauti na watanzania wengi walivyotaraji, goli la dakika ya 76 la Nkau Lerotholi linadumu mpaka sekunde ya mwisho na kuwapa wenyeji Lesotho ushindi wa 1-0 nyumbani na kufufua matumaini yao ya kufuzu AFCON 2019.
Tanzania sasa imeshuka kutoka nafasi ya pili mpaka ya tatu wakiwa na pointi 5 sawa na Lesotho ambao wao wapo nafasi ya pili huku nafasi ya mwisho wakiwa Cape Verde na pointi 4.
Nafasi ya Tanzania kwenda AFCON 2019 inabaki katika mechi ya mwisho dhidi ya Uganda Machi 2019 itakayochezwa nchini Tanzania, huku wakiombea Lesotho asipate pointi 3 dhidi ya Cape Verde kwenye mechi yao ya mwisho.