Harry Kane kuifuta rekodi ya Rooney England
Februari 13,2003 alipokuwa akicheza mechi yake ya kwanza akiwa na jezi ya timu ya Taifa ya England, kichwani kwake hakuwa na wazo kubwa la kuwa mfungaji wa muda wote wa timu hiyo, ni furaha tu ndio ilitawala kwa kutimiza ndoto yake ya kulichezea taifa lake.
Miaka 15 baadae anafikisha mechi 120 akiwa na jezi ya timu hiyo, kikubwa zaidi ni kufunga magoli 53 na kuwa kinara wa magoli wa muda wote wa Taifa lake.
Huyo si mwingine, Wayne Rooney ambaye wiki hii amecheza mechi ya kuagwa katika timu ya Taifa ya England.
Februari 13,2003 Harry Kane alikuwa na umri wa miaka 10 tu wakati akiwa nyumbani kwao akimuangalia Wayne Rooney akicheza mechi yake ya kwanza katika timu ya taifa.
Leo hii Harry amepigania ndoto na sasa ni mchezaji wa kutegemewa katika kikosi cha ile timu ambayo Wayne Rooney ameweka rekodi ya ufungaji.
Kane sasa hana miaka 10 tena, ana umri wa miaka 25 na tayari ameshaweka nadhiri ya kuifikia na kuivunja rekodi hiyo ya Wayne Rooney.
Mpaka sasa Harry Kane amefunga magoli 19 katika timu ya taifa ya England na bado ana muda mrefu wa kufunga magoli zaidi.
“ Bila shaka inawezekana “ Kane alijibu alipoulizwa kuhusu kuvunja rekodi ya Wayne Rooney.
‘ Tutaona baada ya miaka magoli mangapi nitakuwa nayo. Ninatumaini nitakuwa fiti na afya na kocha ataendelea kunichagua ‘
‘ Inafikika lakini si kitu ambacho ninakiwaza sana kwa sasa ‘
Timu ya taifa ya England leo Novemba 18 itakuwa Wembley kuwakaribisha Croatia katika mchezo wa Uefa Nations League. Mchezo huu England wanataka kulipa kisasi cha kutolewa na Croatia katika hatua ya nusu fainali kwenye michuano ya kombe la Dunia mwaka huu nchini Russia.
Endapo England atashinda watakuwa wamepata nafasi ya kuongoza kundi lake na kufuzu hatua za mwisho za Uefa Nations League na wakipoteza watashuka daraja kutoka League A kwenda League B.